BRAZIL 2014

Pamoja kwa Umoja

Wednesday, October 22, 2014

AFRICA NEWS: OSCAR PISTORIUS AFUNGWA MIAKA MITANO
RIADHA
PRETORIA: JAIZMELALEO
Mwanariadha wa Afrika Kusini Oscar Pistorius amehukumiwa kwenda jela kwa miaka mitano kwa mauaji ya mpenzi wake Reeva Steenkamp. 

Jaji Thokozile Masipa, akitoa hukumu hiyo mjini Pretoria, pia amempa kifungo cha nje cha miaka mitatu kwa shtaka la kufyatua silaha. Pistorius amepelekwa moja kwa moja gerezani.

Upande wa mashtaka ulitaka mwanariadha huyo kupewa kifungo cha miaka 10. Upande wa utetezi ulitaka apewe adhabu ya huduma kwa jamii na kifungo cha nyumbani.
 
Pistorius alikutwa na hatia na kumuua bila kukusudia mpenzi wake, na kufutiwa mashtaka ya mauaji.

IPC imethibitisha kuwa mwanariadha huyo hatashiriki michuano yoyote hadi mwaka 2019.

UCL NEWS: MABAO 40 YAFUNGWA, LUIZ ADRIANO ATUPIA MATANO, NEYMAR, MESSI , DROGBA,GERVINHO WAFUMANIA NYAVU, BAYERN YAIKAANGA AS ROMAMICHEZO
 
Mabao 40 yamefungwa jana katika mechi za klabu bingwa barani Ulaya huku kukishuhudiwa vichapo vya hatari vikitolewa kwa timu, Bayern Munich wakishinda 7-1 dhidi ya AS Roma, Shakhtar wakimdabua BATE mabao 7-0, huku Luiz Adriano wa Shakhtar akitupia mabao matano na kuweka rekodi nyingine katika Klabu Bingwa barani humo.


Mechi nyingine Barcelona walishinda kibishi dhidi ya Ajax 3-1, Chelsea wakiizabua NK Maribor mabao 6-0, Schalke wakipata ushindi wa pili chini ya Kocha Di Matteo wa mabao 4-3 walipowakaribisha Sporting CP.

Manchester City walilazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya PFC CSKA Moskva, PSG wakishinda kiduchu dhidi ya APOEL walipoalikwa nchini Cyprus, na Mabingwa wa UCL 2004 FC Porto wakijipoza dhidi ya Athletic Bilbao walipowalaza kwa mabao 2-0.
Kuona majina ya wafungaji bofya hapa chini

Tuesday, October 21, 2014

UCL NEWS: REAL MADRID KULIPA KISASI CHA MWAKA 20008/09Mchakamchaka wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya unaendelea kwa miamba ya soka kushuka viwanjani kutafuta alama muhimu ya kusonga mbele katika hatua ya 16. 

Atletico Madrid itawakaribisha Malmo FF, Juventus wakiwa ugenini dhidi ya Olympiacos, Ludogorets watawaalika Basel 1893 jijini Sofia , Liverpool dhidi ya Real Madrid pale Anfield.

Andres-Vilas Boaz atakuwa na kibarua kigumu ugenini atakapoipeleka Zenith St. dhidi ya Bayer Leverkusen, wakati huo huo Monaco ikiwakaribisha Benfica.

Arsenal itakuwa ugenini dhidi Anderlecht ikitaka kurekebisha makosa baada ya wikiendi kulazimishwa sare na Hull City, Galatasaray itawaalika Dortmund jijini Instabul.
Kabla ya kupiga hatua katika mechi za leo, tuangazie timu zinazoshuka katika viwanja mbalimbali, zilifanya nini mwishoni mwa juma katika michuano ya kwao. 

KUNDI A
Hili lina timu za Club Atletico de Madrid, Juventus, Malmo FF na Olympiacos ambapo kulishuhudiwa Atletico Madrid ikiendeleza rekodi ya kutofungwa nyumbani pale ilipomdabua Espanyol kwa kichapo cha mabao 2-0 katika La Liga.

Juventus waliambulia alama moja baada ya kutoka sare ya 1-1 na Sassuolo Calcio katika Serie A, shukrani zikimwendea Paul Pogba aliyetupia bao hilo.

Malmo FF walipoteza mtanange dhidi ya IF Elfsborg walipokubali kichapo cha mabao 2-1 ukiwa ni mchezo wa kwanza kutetea taji msimu huu.

Olympiacos iliponea chupuchupu kupoteza mtanange dhidi ya Ergotelis, pongezi kwa Kostas Mitroglou aliyetupia bao la ushindi wakiwapotezea kwa kichapo cha mabao 3-2.

KUNDI B
Katika kundi hili, Real Madrid waliinyuka Levante mabao 5-0, Cristiano Ronaldo akitupia mara mbili na kuweka rekodi mpya katika La Liga akiwa ametupia mabao 15 katika mechi nane za kwanza.

Nyota wa FC Basel Shkelzen Gashi alitupia bao lake la tano msimu huu akiiwezesha klabu hiyo kuondoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Young Boys.

Liverpool watapaswa kumshukuru Steven Caulker kwa bao lake la kujifunga wakishinda kwa taabu dhidi ya QPR mabao 3-2 yaliwawezesha The Reds kuchukua pointi muhimu, huku mabao manne ya mechi hiyo yakifungwa katika dakika tatu za mwisho.

Ludogorets Razagrad waliwanyuka FC Haskovo kwa kichapo cha mabao 3-1, Marcelinho aliisawazishia klabu hiyo. 

KUNDI C
AS Monaco waliwanyuka Evian Thonon Gaillard mabao 2-0, juhudi ziwaendee Joao Moutinho na Yannick Ferreira-Carrasco waliotupia mabao hayo.

Zenith imebakia kuwa klabu pekee msimu huu mpaka sasa kwa kutofungwa katika Russia Super League walipotoka sare ya 2-2 na Krasnodar, mabao ya Javi Garcia na Mbrazil Hulk.

Leverkusen waliduwazwa na VFB Stuttgart baada ya kutoka sare ya 3-3 huku wakipata uongozi wa mabao matatu yao katika dakika 10 za kwanza.

Benfica waliishushia kichapo SC Covilha cha mabao 3-2 katika Portuguese Cup huku mbrazili Jonas akitupia hat trick.

KUNDI D
Ilkay Gundogan (Dortmund) alirudi dimbani tena baada ya miezi 14 ya kuwa majeruhi huku akishuhudia mwanzo mbaya walipopoteza dhidi ya FC Koln walipopokea kichapo cha mabao 2-1.

Alexis Sanchez (Arsenal) alitupia bao la kwanza huku Danny Welbeck akiisawazishia dhidi ya Hull City katika EPL, Galatasaray waliwanyuka mahasimu wao Fenerbahce SK wakiwa wamebakia 10 dimbani kichapo cha mabao 2-1 jijini Instabul, makofi tafadhali yamwendee Wesley Sneijder aliyetupia mawili.

RSC Anderlecht waliendeleza rekodi yao ya kutofungwa katika mchezo wa 11 kwenye ligi kuu nchini Ubelgiji  wakitoka sare ya 1-1 KV Mechelen, Steven Defour akiisawazishia Anderlecht.

Baada ya kuangazia mechi za mwishoni mwa juma kwa wanaozama viwanjani leo, tupitie kwa ufupi hii.

MECHI KALI

LIVERPOOL v REAL MADRID
Hapa mtoto haendi kwa jirani kwa maana itakuwa usiku”, Liverpool iliinyuka Real Madrid kwa uwiano wa mabao 5-0 katika hatua ya 16, msimu wa 2008/09 wakati huo The Red’s walikuwa chini ya Rafa Benitez wakishinda 1-0 Santiago Bernabeau na kuwapa kichapo Los Blancos ambacho kimebakia kumbukumbu cha mabao 4-0 Anfield.


Steven Gerrard atakumbukwa sana usiku ule kwani alitupia mawili na kipindi hicho Alvaro Arbeloa alikuwa akiitumikia Merseyside, wakati huo Cristiano Ronaldo alikuwa akimalizia zama zake Manchester United.

Kichapo hicho, Real Madrid walikwenda nacho, vichwa chini wakati huo langoni alikuwepo Iker Cassillas na kufanya kuwa kichapo kikubwa kukipata katika UEFA Champions League wengine waliocheza siku hiyo Sergio Ramos, Fabio Cannavaro, (Van der Vaart 64), Pepe, Gabriel Heinze, Arjen Robben (Marcelo 46), Lassana Diarra, Gago (Guti 77), Wesley Sneijder, Raúl Gonzalez, Gonzalo Higuaín.

Kwa upande wa Liverpool, langoni alisimama Pepe Reina ambaye hakuruhusu bao hata moja katika kipute hicho wengine waliokaza siku hiyo Martin Skrtel, Jamie Carragher, Fabio Aurelio, Xabi Alonso (Lucas 60), Javier Mascherano, Dirk Kuyt, Steven Gerrard (Spearing 73), Babel, Fernando Torres (Dossena 84).

Nafikiri Xabi Alonso atakuwa anatamani angekuwepo kabla hajauzwa kwenda Bayern Munich msimu huu akaonane na Steve G, pia Martin Skrtel, lakini si haba Alvaro Arbeloa atamwakilisha, Liverpool kwa walivyocheza mwishoni mwa wiki dhidi ya QPR, sijuiiiiiiiiiiii!!!!

Aidha Liverpool ilishawatungua Los Blancos katika fainali mwaka 1981 kwa bao pekee la Alan Kennedy, fainali hiyo ya vilabu bingwa barani humo ilichezwa Jijini Paris katika uga wa Parc des Princes.

HEBU CHUNGULIA HII
Kocha wa sasa wa Real Madrid akiwa na AC Milan alinyukwa na Liverpool kwa mikwaju ya penati walipolazimishwa sare ya 3-3 wakati walikuwa wakiongoza 3-0 katika fainali ya mwaka 2005 kabla ya kushinda katika mtanange kama huo mwaka 2007 kwa kuwapa kichapo cha mabao 2-1.

Carlo Ancelotti, akiwa kocha wa Chelsea alikutana na Liverpool mara nne katika EPL akifanikiwa kushinda michezo miwili (2009/10) na kugagaduliwa mitanange miwili (2010/11).

Chicharito ametupia mara mbili katika mara tano alizocheza katika uga wa Anfield akiwa na Manchester United, na bao lake la kukumbukwa dhidi ya Liverpool, Old Trafford ni lile la September 2013 katika kikombe cha ligi.

Cristiano Ronaldo ametupia mara mbili katika mechi tisa alizocheza dhidi ya Liverpool akiwa na Manchester United, wakishinda mara tano, sare moja na kufungwa tatu.

Luka Modric ameikabili Liverpool akiwa na Tottenham mara nane wakishinda mara tano, kupoteza mbili na sare moja huku akitupia katika ushindi wa 2-0 pale Anfield Mei 2011.

Gareth Bale ameikabili Liverpool akiwa na Spurs wakishinda mara nne, sare mbili na kupoteza tatu, akibakiwa na kumbukumbu ya bao lake moja katika mechi tisa alizoikabili Liverpool waliposhinda 2-1 Novemba 2012.

Mario Balotteli alikuwepo katika kikosi cha Italia walipokaangwa mabao 4-0 na Hispania EURO 2012 , ndani yake walikuwepo Cassilas, Arbeloa, Ramos ambao anakutana nao tena.

Nihitimishe kwa hili, hawa hucheza pamoja katika timu zao za taifa Coutinho, Lucas and Marcelo (Brazil); Dejan Lovren na Modrić (Croatia); Mamadou Sakho, Raphaël Varane and Karim Benzema (Ufaransa); Joe Allen na Bale (Wales).
 
Etou brevement!!!!

Imetayarishwa na:
Jabir Johnson,
Blogger & Photo Journalist
+255- (0)-768 096 793

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

G


website counters

BLOGU NYINGINE

TOPSy KRETTS

TOPSy KRETTS

KONA YA PRO

KONA YA PRO